Katika makala haya ni maelezo kuhusu Fomu ya Ombi la Cheti Mbadala NECTA – Baraza la Mitihani Tanzania jinsi ya kupata cheti mbadala, jinsi ya kuomba cheti kingine necta, hatua za kufata wakati umepoteza cheti chako iwe ni cha darasa la saba, kidato cha nne au kidato cha sita. Endelea kusoma hapa chini.
FOMU YA OMBI LA CHETI MBADALA (REPLACEMENT CERTIFICATE)
- UTARATIBU WA MAOMBI
Soma maelekezo yafuatayo kabla ya kujaza fomu hii:-
- Hakikisha kwamba taarifa utakazoandika katika fomu hii ni sahihi. Iwapo tarifa uliyoandika haitakuwa sahihi, cheti mbadala hakitaandaliwa.
- Gharama ya cheti mbadala ni Tsh. 100,000/=
- Ombi la cheti mbadala litapokelewa baada ya miezi mitatu (03) kupita tangu kutangazwa gazetini kwa upotevu wa cheti cha awali.
- Mchakato wa uchunguzi utafanyika katika kipindi cha siku thelathini (Mwezi mmoja) tangu kupokelewa kwa ombi la cheti mbadala ambapo Jeshi la Polisi (Kitengo cha uchunguzi wa picha) litahusika katika kukamilisha uchunguzi huo.
- Cheti mbadala kitatolewa mara moja tu na kitakabidhiwa kwa mtahiniwa mwenyewe na si vinginevyo.
- Iwapo cheti kilichopotea kitabainika kutumika katika soko la ajira au mafunzo na mtahiniwa akabainika kushiriki katika kulidanganya Baraza la Mitihani katika kumwezesha mtumiaji wa cheti hicho kukitumia wakati sio chake, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu wote waliohusika katika udanganyifu huo.
- Hakikisha kwamba unavyo viambatisho vifuatavyo:-
- Iwapo cheti kimepotea, tangazo la gazeti la upotevu wa cheti (taarifa muhimu kwenye tangazo hilo ni Jina la mtahiniwa, Namba ya mtihani, aina ya mtihani, mwaka wa mtihani, jina la shule, picha ya mtahiniwa na mahali cheti kilikopotea), Hati ya polisi ya upotevu wa cheti, Picha (Passport size) utakayobandika kwenye fomu ya ombi la cheti mbadala, Nakala ya kitambulisho na Risiti halisi ya malipo au “Control Number”.
- Iwapo cheti chako kiliungua moto, kuharibiwa na mchwa, mafuriko, panya au kwa namna nyingine yoyote hutatakiwa kutangaza gazetini juu ya uharibifu huo bali utawasilisha vielelezo vilivyotajwa hapo juu pamoja na barua ya serikali ya mtaa wa eneo la tukio la moto au mafuriko yalipotokea. Iwapo yapo mabaki ya cheti husika utatakiwa kuwasilisha mabaki hayo Baraza la Mitihani la Tanzania.
- Baada ya kukamilisha ujazaji wa fomu na malipo, tafadhali tuma au wasilisha fomu yenye viambatisho vilivyotajwa kwa Katibu Mtendaji, Baraza la Mitihani la Tanzania, S.L.P 2624, Dar es Salaam.
- Malipo kwa ajili ya huduma ya cheti mbadala yafanyike kwa kutumia namba maalum (Control
Number) inayotolewa na mfumo wa malipo ya serikali wa kielektroniki (GePG) kupitia tovuti ya NECTA: http://www.necta.go.tz au piga simu namba +255-22-2700493…6 kwa msaada zaidi. Malipo yote yafanyike katika benki za: NMB; CRDB na NBC au kwa kutumia mitandao ya kifedha ya M-Pesa na Tigo Pesa.
Bonyeza hapa kudownload Fomu ya ombi la cheti mbadala kutoka NECTA
Endelea kusoma maelezo chini..
Jinsi ya kuomba cheti mbadala NECTA – Baraza la Mitihani Tanzania.
MASHARTI YA KUOMBA CHETI MBADALA:
Mwombaji wa cheti mbadala unatakiwa kutimiza masharti yafuatayo:-
(a) Uwe ni mtahiniwa halisi uliyefanya mtihani na kutunukiwa cheti cha awali chenye picha kisha kikapotea, kuharibika au kuungua moto.
(b) Uwe mkweli, mwaminifu na mwenye dhamira ya kweli ya hitaji la cheti mbadala baada ya kutokuwa na cheti cha awali kwa sababu ya matukio yaliyotajwa katika kipengele (a) hapo juu.
(c) Picha yako itafananishwa na picha iliyotumika kufanya mtihani husika. Iwapo picha hizo hazitafanana, uchunguzi utafanyika ili kubaini ukweli wa tofauti hizo. Aidha, iwapo matokeo ya uchunguzi yatabaini kuwa aliyefanya mtihani huo ni mtahiniwa tofauti na wewe, basi itakuwa imethibitika kuwa ulikuwa unajaribu kujipatia cheti mbadala isivyo halali kinyume cha sheria. Hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yako.
(d) Cheti mbadala kitatumiwa na mtahiniwa husika tu katika ajira na mafunzo. Iwapo cheti kilichopotea (kwa waliopoteza vyeti) kitapatikana, cheti mbadala kirudishwe Baraza la Mitihani mara moja.
(e) Uwe umetekeleza maelekezo yote yaliyoainishwa katika vipengele (a) hadi (d) hapo juu.