Leo NECTA Tanzania, Wametoa Fomati ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi Darasa la Saba 2024. Kitabu hiki cha fomati ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi kimeandaliwa na Baraza la Mitihani la Tanzania kwa kuzingatia matakwa ya Mtaala wa Elimu ya Msingi wa mwaka 2015. Fomati hii itaanza kutumika mwaka 2024.
Katika kitabu hiki cha Fomati kuna maboresho ya idadi ya sehemu za karatasi hususani katika masomo ya 03 Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, 04 Hisabati, 05 Sayansi na Teknolojia na 06 Uraia na Maadili ambapo kutakuwa na sehemu tatu (03) A, B na C badala ya mbili (2) za awali ambazo ni A na B. Maboresho zaidi yaliyofanyika katika muundo wa mtihani wa masomo yote yanayotahiniwa katika ngazi hii ya elimu ambayo ni 01 Kiswahili, 02 English Language, 03 Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, 04 Hisabati, 05 Sayansi na Teknolojia pamoja na 06 Uraia na Maadili. Muundo wa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi utakuwa na idadi ya maswali ambayo ni tofauti kutoka somo moja hadi jingine ikilinganishwa na idadi ya awali ambapo masomo yote yalikuwa na maswali 45. Katika maboresho hayo masomo ya 01 Kiswahili na 06 Uraia na Maadili yatakuwa na maswali sita (6) kila moja. Masomo ya 04 Hisabati na 05 Sayansi na Teknolojia yatakuwa na maswali nane (8) kila moja. Aidha, masomo ya 02 English Language na 03 Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi yatakuwa na maswali saba (7) kila moja. Katika mitihani hiyo mtahiniwa ataandika majibu yake kwenye nafasi zilizotengwa katika karatasi ya maswali.
FOMATI YA DARASA LA SABA NECTA – KUMALIZA ELIMU YA MSINGI 2024
Fomati za mtihani zimeandaliwa kwa kufuata muundo wa sehemu tano ambazo ni Utangulizi, Malengo ya Jumla, Umahiri Mkuu, Muundo wa Mtihani na Umahiri utakaotahiniwa kwa kila somo. Aidha, Jedwali la utahini limewekwa mwishoni mwa fomati ya kila somo na linaonesha umahiri utakaopimwa, ngazi za nyanja ya utambuzi, idadi ya vipengele vya maswali kwa kila umahiri mahususi na asilimia ya uzito kwa kila umahiri.
Kwa ujumla, kitabu hiki cha fomati kinatoa mwongozo kwa watunzi wa mitihani, warekebishaji wa maswali ya mtihani na walimu wa shule za msingi katika kuandaa mitihani inayozingatia haki, uhalali na viwango. Baraza linasisitiza umahiri wote katika masomo yote yanayofundishwa katika ngazi ya elimu ya msingi ufundishwe kwa kuzingatia mihtasari ya masomo husika. Fomati hii ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi kwa namna yoyote ile isitumike kama mbadala wa mihtasari ya masomo husika. Baraza la Mitihani linatambua na kuthamini mchango wa watu wote walioshiriki katika kufanya maboresho ya kitabu hiki cha fomati.