TANGAZO LA UFADHILI WA KUJIENDELEZA KWA WATUMISHI WA UMMA KADA ZA AFYA KUPITIA ‘DKT SAMIA HEALTH SPECIALIZATION SCHOLARSHIP PROGRAM’ KWA MWAKA 2024/2025
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Afya nchini kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya zikiwemo huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi hapa nchini. Uwekezaji katika Sekta ya Afya kwenye ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kutoa huduma za afya, ajira za wataalamu wa afya, ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi unatakiwa kwenda sambamba na kuendeleza wataalamu wa afya ili waweze kutoa huduma bora za matibabu ikiwemo ya matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi kwa wananchi.
Ufadhili wa Watumishi Kada ya Afya
Katika kufanikisha azma ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha huduma za kibingwa na kibobezi nchini, Wizara ya Afya imejiwekea lengo la kusomesha wataalamu wapya wa afya wasiopungua 300 katika ngazi za ubingwa na ubingwa bobezi kwa kila mwaka wa fedha kupitia Mpango wa Ufadhili unaojulikana kama Dkt Samia Health Specialisation Scholarship Program in Tanzania. Hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anawatangazia watumishi wote waliopata udahili wa kusoma masomo ya Shahada ya Uzamili katika fani za afya kwa mwaka 2024/2025 kwamba Dirisha la Maombi ya Ufadhili wa Masomo kupitia Dkt Samia Health Specialization Scholarship Program 2024 limefunguliwa. Wizara itaanza kupokea maombi ya ufadhili kuanzia tarehe 09/08/2024 hadi tarehe 31/08/2024. Maombi hayo yatawasilishwa kwa njia ya kielektroniki kwa kutumia ‘link‘ iliyotolewa kwenye tangazo hili. Maombi yatakayofanyiwa kazi ni yale yatakayowasilishwa kwa njia ya mfumo huo tu. Hivyo, waombaji waliowasilisha maombi yao kabla ya tangazo hili wanapaswa kufuata utaratibu huu.
Bonyeza hapa kudownload tangazo la udahili kwa watumishi wa Umma kada za Afya
Aidha, mwombaji atatakiwa awe ameambatisha nakala halisi za nyaraka zifuatazo wakati wa kufanya maombi ya ufadhili wa kujiendeleza kada ya Afya 2024/2025: –
a. Barua ya ruhusa kwenda masomoni kutoka kwa mwajiri wake.
b. Barua ya udahili kutoka chuoni.
c. Cheti cha taaluma cha sasa (current academic qualification).
d. Cheti cha usajili na leseni hai kutoka kwenye Baraza la taaluma husika.
e. Cheti cha kuzaliwa.
f. Kitambulisho cha Taifa (NIDA).
Maombi yote yawasilishwe kwa kutumia ‘link’ ifuatayo: https://esponsorship.moh.go.tz/
MUHIMU: Kama ilivyoelekezwa hapo juu, mwisho wa kupokea maombi haya ni tarehe
31/08/2024.
Imetolewa na: –
KATIBU MKUU,
WIZARA YA AFYA,
Mji wa Serikali Mtumba,
Barabara ya Afya,
S.L.P 743,
40478 DODOMA.
09/08/2024
Vigezo vitakavyotumika kuwapata watakaofadhiliwa Ufadhili wa watumishi kada za afya ni kama ifuatavyo: –
1. Kuwasilishwa kwa maombi rasmi ya ufadhili kwa njia ya mfumo (Post-graduate Sponsorship Online Application System).
2. Mwombaji awe ni Raia wa Tanzania.
3. Awe mtumishi wa Serikali.
4. Awe ana barua ya udahili (admission letter) kutoka kwenye chuo kinachotambuliwa na Serikali ndani au nje ya nchi.
5. Awe anakwenda kusoma masomo ya ubingwa (specialization) au ubingwa bobezi (super-specialization).
6. Mwombaji awe ametimiza miaka mitatu tangu alipoajiriwa (barua ya ajira na kuthibitishwa kazini iambatishwe wakati wa maombi).
7. Ufadhili utazingatia uhitaji unaotokana na uhaba wa taaluma/fani anayokwenda kusoma mtumishi kwenye kituo husika. Kwa mantiki hiyo, kipaumbele cha kupata ufadhili itategemea upungufu wa taaluma aliyoomba kwenda kusoma kwenye kituo chake cha kazi.
UFADHILI WA WATUMISHI WA UMMA KADA YA AFYA 2024 – DKT SAMIA HEALTH SPECIALIZATION SCHOLARSHIP PROGRAM
Wataalamu watakaopata ufadhili wa masomo kwa vyuo vya nje ya nchi watalipiwa ada ya mafunzo, posho ya kujikimu, nauli pamoja na posho ya utafiti. Wataalamu watakaopata ufadhili masomo katika vyuo vya ndani ya nchi watalipiwa ada ya mafunzo na posho ya utafiti pindi mtaalamu husika atapokuwa kwenye kipindi cha kufanya utafiti kama sehemu ya mafunzo yake. Malipo ya posho ya utafiti na posho ya kujikimu yatazingatia viwango vilivyopangwa na Wizara.