KUFUNGULIWA KWA DIRISHA LA UDAHILI KWA WAOMBAJI WA SHAHADA YA KWANZA KATIKA TAASISI ZA ELIMU YA JUU NCHINI TANZANIA KWA MWAKA WA MASOMO 2024/2025
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inapenda kufahamisha umma, Taasisi za Elimu ya Juu na Wadau wote wa Elimu ya juu ndani na nje ya nchi kuwa dirisha la maombi ya udahili kwa waombaji wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2024/2025 limefunguliwa kuanzia leo tarehe 15/7/2024. Dirisha hili litakuwa wazi hadi tarehe 10/8/2024.
Tume inatoa wito kwa waombaji wote wa Shahada ya Kwanza, endapo watahitaji kupata ufafanuzi wa suala lolote linalohusu udahili, wawasiliane moja kwa moja na vyuo husika. Aidha, iwapo watahitaji maelezo ya jumla wanaweza kuwasiliana na TCU kwa kutumia barua pepe es@tcu.go.tz.
Pia, TCU inawaasa wananchi kuepuka kutapeliwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma za jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini.
Masuala Muhimu ya Kuzingatiwa na Waombaji Udahili TCU
a) Kusoma kwa makini na kuelewa mwongozo wa udahili uliotolewa na TCU pamoja na maelekezo mahsusi ya vyuo kabla ya kuanza kutuma maombi ya udahili.
b) Kuingia katika tovuti za vyuo na kuwasiliana na vyuo moja kwa moja ili kujua taratibu za kutuma maombi na kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo ili kujiandikisha kabla ya kutuma maombi.
c) Kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielekroniki iliyowekwa na vyuo husika.
d) Waombaji wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani nje ya nchi wanapaswa kuwasilisha vyeti vyao katika Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kwa vyeti vya Elimu ya Sekondari au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa vyeti vya Stashahada ili kupata ithibati ya ulinganifu wa sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili.
Tume inawahimiza waombaji wote wa udahili kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia tovuti ya TCU http://www.tcu.go.tz , tovuti za vyuo vilivyohusika kudahili wanafunzi wa Shahada ya Kwanza, pamoja na taarifa mbalimbali zinazotolewa na TCU kupitia vyombo vya habari.
Vigezo na Sifa za Waombaji Udahili
Vigezo na sifa katika programu mbalimbali za masomo vinapatikana katika tovuti za vyuo husika na katika vitabu vya mwongozo wa maombi ya udahili vinavyopatikana katika tovuti ya TCU http://www.tcu.go.tz
Utaratibu wa Kutuma Maombi ya Udahili TCU
a) Maombi yatumwe moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo mwombaji amevichagua kwa kuzingatia programu za masomo anazozipenda.
b) Maelekezo mahsusi ya jinsi ya kutuma maombi yanatolewa na vyuo husika.
JINSI YA KUTUMA MAOMBI YA UDAHILI TCU 2024/2025
UTARATIBU WA MAOMBI YA UDAHILI KWA MWAKA WA MASOMO 2024/2025
Makundi ya Waombaji wa Udahili
Maombi ya udahili wa kujiunga na Shahada ya Kwanza yanahusisha makundi matatu ya waombaji:
a) Wenye sifa stahiki za Kidato cha Sita;
b) Wenye sifa stahiki za Stashahada (Ordinary Diploma), au sifa linganifu;
c) Wenye sifa stahiki za Cheti cha Awali (Foundation Certificate) cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Ili kufahamu sifa stahiki kwa makundi matatu yaliyotajwa hapo juu, vyuo na programu zilizoidhinishwa kudahili, waombaji wanapaswa kusoma vigezo vilivyooneshwa katika vitabu vya mwongozo wa maombi ya udahili vinavyotolewa na TCU (Bachelor’s Degree Admission Guidebooks for 2024/2025 Academic Year) vinavyopatikana katika tovuti ya TCU http://www.tcu.go.tz