Utaratibu wa Malipo ya Mkopo HESLB; Gharama za chakula na malazi, vitabu na viandikwa, mafunzo kwa vitendo, gharama za tafiti yatalipwa moja kwa moja kwa mwanafunzi wakati Ada ya mafunzo na mahitaji maalum ya kitivo yatalipwa moja kwa moja kwenye taasisi husika ya elimu ya juu.
Ikitokea mwanafunzi hajasaini kwa wakati, mkopo utarejeshwa HESLB baada ya siku 30 kutoka tarehe ambayo mnufaika alilipwa. Kiasi kilichorejeshwa hakitarudishwa kwa mwanafunzi na hakitakuwa sehemu ya deni lake. Malipo yoyote yatakayofuata lazima kuwe na uthibitisho kutoka chuoni.
Orodha ya Waombaji Waliochaguliwa / waliopangiwa kwenye Taasisi za Elimu ya Juu
HESLB itazingatia maombi ya mkopo kutoka kwa wanafunzi waliodahiliwa katika Taasisi za Elimu ya Juu na kuthibitishwa na kuwasilishwa HESLB na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) au mamlaka nyingine iliyothibitishwa.
KUHAMA CHUO AU KOZI NDANI YA CHUO
HESLB haitafanya malipo ya mkopo kwa wanafunzi ambao watahama vyuo kwa hiari yao wenyewe. Baada ya kupokea uthibitisho wa uhamisho wa mwanafunzi kutoka kwa mamlaka husika, uhamisho wa mkopo utafanyika. Hakuna uhamisho wa mkopo utakaofanyika zaidi ya siku mia moja ishirini (120) baada ya kutangazwa taarifa za udahili. Uhamisho wa mkopo utafanyika kulingana na kiasi cha mkopo kilichopangwa awali.
UREJESHAJI MKOPO HESLB
Baada ya kuhitimu au kusitisha masomo ya elimu ya juu, mnufaika wa mkopo atatakiwa kurejesha mkopo kwa makato si chini ya asilimia kumi na tano (15%) ya mshahara wake wa kila mwezi. Mnufaika ambaye amejiajiri anapaswa kurejesha mkopo wake kwa kiwango kisichopungua shilingi laki moja (100,000/=) kwa mwezi au 10% ya pato lake linalotozwa kodi. Mikopo yote inatozwa asilimia moja (1%) ya ada ya uendeshaji kwenye mkopo halisi wa mnufaika kwa mwaka.